LIONEL MESSI APIGA HAT-TRICK MARA 19, MAGOLI MANNE @ MECHI MARA 3, MABAO MATANO @ MECHI MARA 1

 
LIONEL Messi, ambaye alikuwa shujaa wa 
mechi ya ugenini ya Barcelona dhidi ya Deportivo kwenye Uwanja wa 
Riazor, amefunga magoli matatu au zaidi mara 23 katika maisha yake ya 
soka, huku 21 kati ya hizo akiwa na Barcelona na mara mbili akiwa na 
timu yake ya taifa ya Argentina.
Katika mechi hizo 23, amefunga 
'hat-trick' mara 19. Katika mechi tatu kati ya nne zilizobaki alipiku 
rekodi zake mwenyewe kwa kufunga magoli manne dhidi ya Arsenal, Valencia
 na Espanyol na katika mechi nyingine moja 'akajifunika' kabisa mwenyewe
 kwa kufunga magoli matano dhidi ya Bayer Leverkusen mwaka huu katika 
mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Akizungumzia ushindi wa timu
 yake wa 5-4 dhidi ya Deportivo ambapo yeye alifunga 'hat trick', Messi 
alisema: "Tumeshinda. Daima inakuwa ngumu sana kucheza mechi tukitokea 
kuziwakilisha timu zetu za taifa, kwasababu unarejea ukiwa umechoka. Huu
 ulikuwa ni ushindi muhimu," alisema.
'Supastaa' huyo wa 
Argentina alisema kutokea uwanjani hakuona kama Deportivo walistahili 
penalti wala kutolewa kwa kadi nyekundu kwa Mascherano. "Sikuona jambo 
lile. niliambiwa kwamba haikutahili kuwa penalti wala kadi nyekundu, 
lakini hivyo ndivyo ilivyotokea na refa akaona kinyume," alisema.
Aidha,
 Messi alipuuza 'hat-trick' aliyofunga pamoja na magoli 59 aliyofunga 
katika mwaka 2012, ambayo ni rekodi kwa mchezaji wa Barcelona. Katika 
mwaka huu wa kalenda kuanzia Januari 2012 hadi sasa, Messi ameifungia 
klabu yake magoli 59 na ameifungia timu yake ya taifa ya Argentina 
magoli 12 na kufanya jumla ya mabao 71, manne tu pungufu ya rekodi ya 
wakati wote inayoshikiliwa na Pele aliyefunga magoli 75 mwaka 1959. 
Messi anatarajiwa kuivunja rekodi hiyo na kuweka yake ya hatari zaidi 
kwani bado ana zaidi ya miezi miwili ili mwaka huu 2012 umalizike 
Desemba 31.
"Tunachopaswa kufanya ni kuendelea kushinda, kucheza 
katika kiwango tulichokuwa nacho kabla ya mapumziko ya kwenda 
kuzitumikia timu zetu za taifa. Takwimu za 'hat-trick' si muhimu, 
kushinda mechi zetu ndiyo muhimu, pamoja na kuchangia mafanikio ya 
klabu," alisema.